Kaunti ya Trans Nzoia imepokea shehena ya kwanza ya mbolea ya bei nafuu kutoka kwa serikali kuu wakati msimu wa upanzi ukikaribia.
Wakulima wa eneo hilo wameombwa kutembelea ghala ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) mjini Kitale na kujiandikisha mapema ili kuepuka changamoto za msongamano dakika za mwisho.
Kamishna wa Kaunti ya Trans Nzoia Gideon Oyagi alisema mbolea hiyo inakusudiwa kupunguza gharama ya uzalishaji na kuongeza uzalishaji na usalama wa chakula.
Akiongea katika ghala ya mji wa Kitale wakati wa kupokea shehena hiyo ya mifuko 2,880 ya kilo 50, Oyagi alisema serikali imejitolea kuhakikisha kuwa Wakenya hawasumbuliwi na makali ya njaa.
Aliongeza kuwa serikali ya Rais William Ruto inalenga kuona kuwa taifa hili lina chakula cha kutosha ili liweze kujilisha na pia kuuza chakula nje ya nchi.
“Hii ndio maana mbolea ya bei nafuu ilitolewa ili kupiga jeki uzalishaji wetu wa chakula,” alisema Oyagi.
Mwenyekiti wa kamati ya usalama wa kaunti hiyo alitoa onyo kali kwa wakulima ambao wananunua mbolea hiyo kwa lengo la kuiuza kwa minajili ya kupata faida.
Alisema vyombo vya usalama viko ange na watawakamata wale wanaopakia mbolea upya na kuwauzia wakulima bila wao kujua.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo katika kaunti ya Trans Nzoia Phanice Khatundi alisema kuwa serikali ya kaunti itawezesha usambazaji wa mbolea hiyo kwa wakulima mashinani.
Aliwarai wakulima kuchanganya mbolea yenye madini mbalimbali ili kupata mazao mazuri na kuwaonya dhidi ya kulaghaiwa na matapeli wanaouza mbolea ya serikali.
Meneja wa ghala ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao mjini Kitale Milcah Lunani alisema wataanza mara moja kuuza mbolea kwa wakulima ambao wamepokea vyeti vya kujisajili.
“Tunatarajia mbolea zaidi ya kupandia na ya kuongeza rotuba. Tunawahimiza wakulima kujisajili mapema ili wawe na muda unaotosha wa kuandaa mashamba yao,” alisema Lunani.
Aliwaomba wakulima ambao hawajapokea vyeti vyao vya kuchukua mbolea wawe na subira kwani Wizara ya Kilimo inawashughulikia.
Wakulima zaidi ya 100,000 walisajiliwa na Wizara ya Kilimo kwenye kaunti ya Trans Nzoia mwaka uliopita.