Mwanamuziki wa Canada Daystar Shemuel Shua Peterson, maarufu kama Tory Lanez amezungumza kuhusu hatua ya mwanamuziki mwenza Megan Thee Stallion ya kwenda mahakamani kutafuta maagizo ya kumzuia kumkaribia au kuingilia maisha yake kwa vyovyote.
Mawakili wa Lanez wanasema kwamba Megan sio wa kuaminika. Kulingana nao, madai ya binti huyo kwamba Tory aliwasilisha stakabadhi za kisheria kuhujumu filamu yake ya matukio halisi kwenye Amazon Prime ni ya uongo.
Wanasema pia kwamba muda ambao Megan anaashiria wa Tory kuwasilisha stakabadhi hizo hauhusiani kwa vyovyote na uzinduzi wa filamu yake na walifanya hivyo kutimiza tu mahitaji ya kisheria na makataa.
Katika ombi lake kwa mahakama, Megan alidai kwamba Tory anaonekana kana kwamba anataka kuanzisha vita vya kimawazo kwa kutumia wanablogu kumsema vibaya mitandaoni.
Mawakili wa Megan Thee Stallion kwa upande mwingine wanadai kuwa na ushahidi kwamba Tory ana uhusiano na mwanablogu ambaye amekuwa kimtupia maneno .
Anadaiwa kufichua mambo kadhaa juu ya Megan kama vile stakabadhi za malipo ambayo babake Tory anasemekana kutoa kwa mwabamlogu huyo aitwaye Elizabeth Milagro Cooper kati ya Oktoba 2020 na Machi 2022 ya jumla ya dola elfu 3.
Mawakili wa Tory wanasisitiza kwamba malipo hayo hayana uhusiano wowote na Lanez na kwamba ukweli utafahamika mahakamani.
Wanasisitiza kwamba Megan hafai kuaminiwa kabisa hasa baada yake kukiri kumdanganya Gayle King kuhusu kushiriki tendo la ndoa na Tory.
Megan aliwahi kumshtaki Tory kwa kumpiga risasi kwenye mguu, kesi iliyomalizika kwa Tory Lanez kutuhumiwa kwa mashtaka ya kushambulia kwa kutumia bunduki.
Tukio hilo lilitokea Julai 2020, wakati Megan Thee Stallion alipigwa risasi kwenye miguu yake yote baada ya sherehe huko Hollywood Hills.
Alifunua baadaye kuwa Tory Lanez ndiye aliyemshambulia kwa risasi, lakini Tory alikana tuhuma hizo.
Kesi ilifanyika mnamo Desemba 2022, ambapo Lanez alikabiliwa na mashtaka matatu ya uhalifu ambayo ni kushambulia kwa bunduki, kubeba bunduki isiyo na usajili na iliyojazwa risasi na kupiga risasi kwa uzembe mkubwa.
Megan Thee Stallion alishuhudia kuwa Lanez alimpiga risasi baada ya ugomvi kwenye gari.
Baada ya wiki moja ya ushuhuda na majadiliano, kundi la waamuzi lilimpata Tory Lanez na hatia kwa mashtaka yote mnamo Desemba 23, 2022.
Lanez alihukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani Agosti 2023, baada ya kikao cha hukumu. Aidha mawakili wa Lanez waliwasilisha ombi la kukata rufaa mara baada ya hukumu kutolewa.
Kesi hiyo ilivutia vyombo vya habari na umma kutokana na umaarufu wa Lanez katika tasnia ya muziki na mazungumzo mapana kuhusu vurugu, jinsia na haki.
Tory Lanez na Megan Thee Stallion walikuwa na uhusiano wa kimapenzi, ingawa uhusiano wao haukujulikana sana mwanzoni.
Ilikisiwa kwamba walichumbiana au angalau walikuwa na uhusiano wa kimapenzi wa muda mfupi mwaka 2020.
Hata hivyo, uhusiano wao ulijulikana baada ya tukio la Megan kupigwa risasi miguuni.