Tim Scott ajiondoa kwa kinyang’anyiro cha urais nchini Marekani

Tom Mathinji
2 Min Read

Seneta wa chama cha Republican nchini Marekani Tim Scott kutoka South Carolina amejiondoa katika kinyang’anyiro cha urais wa 2024.

Scott alikuwa na matumaini ya kuwa Mwafrika-Mmarekani wa kwanza kupata uteuzi wa chama cha Republican. Ingawa Tim Scott alifadhiliwa vyema, alishindwa kuzoa matokeo bora katika kura za maoni.

Hajaidhinisha mgombea yeyote kati ya waliosalia na alikataa kuwania wadhifa wa makamu wa rais.

Akiwa ameingia kwenye kinyang’anyiro mwezi Mei cha uteuzi wa chama cha Republican, Scott, mwenye umri wa miaka 58, alijidhihirisha kama mgombea mwenye msimamo mkali ambaye angeweza kufanya kazi nzuri ya kuziba nyufa za migawanyiko ya kisiasa ya Marekani kuliko Rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump.

Uamuzi wake wa kujiondoa kwenye kampeni za urais wa chama cha Republican uliwadia muda mfupi baada ya mjadala wa tatu wa urais wiki jana mjini Miami.

Trump, mshiriki wa mbele katika kinyang’anyiro hicho akiwa na uongozi wa juu zaidi ya wapinzani wake wa chama cha Republican, hajashiriki midahalo hiyo ya televisheni.

Scott ni mwaniaji wa pili kutoka kwa hadhi ya juu kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais wa Marekani mwaka 2024.

Aliyekuwa Makamu wa Rais Mike Pence, mwenye umri wa miaka 64, alijiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho mwishoni mwa mwezi Oktoba baada ya kukosa kupata uungwaji mkono kutoka kwa wapiga kura wa chama cha Republican.

Website |  + posts
Share This Article