Tems aandikisha historia kwenye FIFA Club World Cup

Aliteka hisia za mashabiki zaidi ya 80,000 waliokuwepo uwanjani kwa wimbo wake maarufu "Love Me JeJe" .

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki wa asili ya Nigeria Temilade Openiyi maarufu kama Tems aliandikisha historia ya kuwa msanii wa kwanza wa Afrika kuwahi kuongoza tumbuizo la katikati ya mechi ya fainali ya kombe la dunia la vilabu.

Haya yalifanyika katika uwanja wa MetLife ulioko New Jersey nchini Marekani.

Tems alikuwa jukwaani pamoja na wasanii wengine maarufu kama J Balvin na Doja Cat katika onyesho lililoratibiwa na Global Citizen kwa kushirikiana na FIFA.

Tems aliteka hisia za mashabiki zaidi ya 80,000 waliokuwepo uwanjani kwa wimbo wake maarufu “Love Me JeJe” wa albamu yake ya kwanza iitwayo “Born in the Wild”.

Wimbo huu, uliotolewa Aprili 2024, ni tafsiri ya kisasa ya kibao cha Seyi Sodimu cha mwaka 1997 na umemletea Tems tuzo ya Grammy ya “Best African Music Performance” katika Tuzo za Grammy awamu ya 67.

J Balvin alileta ladha ya muziki wa reggaeton, Doja Cat akaonyesha umahiri wake katika pop na hip-hop, huku Coldplay na Emmanuel Kelly wakitoa burudani ya kipekee kwa mashabiki.

Mbali na burudani, onyesho hili lilikuwa na lengo la kijamii ambapo sehemu ya mapato ya tiketi, yameelekezwa kwa hazina ya FIFAya elimu ulimwenguni.

Hazina hiyo inalenga kukusanya dola milioni 100 kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa elimu bora kwa watoto Duniani kote.

Tems ameendelea kuandika historia kimataifa kwa kushinda tuzo ya Grammy, amekuwa Mwanamuziki wa kwanza wa kike kutoka Afrika kushiriki katika Met Gala na aliorodheshwa katika orodha ya Time 100 Next ya mwaka 2023.

Ameonyesha kwamba muziki wa Afrika una nafasi kubwa katika jukwaa la kimataifa.

Website |  + posts
Share This Article