Taiwan imesisitiza kuwa ni taifa huru na lenye mamlaka kamili, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuionya dhidi ya kutangaza rasmi uhuru kutoka China.
Kauli za Trump zilikuja baada ya mkutano wa siku mbili mjini Beijing, ambapo baadaye alisema kwamba hakutoa ahadi yoyote upande wowote, kuhusu kisiwa hicho kinachojitawala.
Kwa muda mrefu China imekuwa ikidai kwamba kisiwa hicho sehemu ya himaya yake na haijaondoa uwezekano wa kukichukua kwa nguvu.
Baada ya mazungumzo na Rais wa China Xi Jinping, Trump pia alisema angeamua hivi karibuni iwapo ataidhinisha mauzo ya silaha za thamani ya dola bilioni 11 za Marekani kwa Taiwan.
Utawala wa Marekani unatakiwa kisheria kuipatia Taiwan uwezo wa kujilinda, lakini mara nyingi umekuwa ukijaribu kusawazisha uhusiano huo huku ukiendelea kudumisha mahusiano ya kidiplomasia na China.
Rais wa Taiwan Lai Ching-te awali alisema kuwa Taiwan haina haja ya kutangaza rasmi uhuru kwa sababu tayari inajiona kama taifa lenye mamlaka kamili.
Jumamosi, msemaji wa rais Karen Kuo alisema ilikuwa “wazi kabisa” kwamba Taiwan ni “nchi ya kidemokrasia, huru na yenye mamlaka kamili”.
Hata hivyo, aliongeza kuwa Taiwan imejitolea kudumisha hali ilivyo katika uhusiano wake na China, ambapo Taiwan haitangazi uhuru kutoka China wala kuungana nayo.
Watu wengi wa Taiwan hujiona kuwa sehemu ya taifa tofauti, ingawa wengi wao wanapendelea kuendelea na hali yao ya sasa.
Msimamo rasmi wa Marekani ni kwamba haiungi mkono uhuru wa Taiwan, huku mahusiano yake ya kuendelea na China yakitegemea kukubalika kwa msimamo kwamba kuna serikali moja tu ya China.