Mwanamuziki wa mtindo wa Hip Hop wa asili ya Kenya Sandra Chebet Koech au Msupa S, amemkumbuka na kumshukuru msanii mwenza Khaliggraph Jones.
Msupa alichapisha picha yake akiwa na Khaligraph ambayo inaaminika kupigwa waliposhirikiana kikazi mwaka 2018 wakati walitoa kibao, “Watajua Hawajui”.
“Kutoka mbali nayo nimetoka, shukrani kwa huyo jamaa ambaye aliamua kunisaidia wakati watu walikuwa wakinicheka,” aliandika Sandra chini ya picha hiyo kwenye Instagram.
Alimalizia kwa kusema kwamba ataendelea kumshukuru Khaligraph au ukipenda OG kila wakati huku akimwombea baraka kwa Mungu.
Msupa S mzaliwa wa kaunti ya Bomet, alipata umaarufu mwaka 2018 kutokana na mtindo wake wa kipekee wa kuchanganya Kiingereza, Kiswahili, na Kalenjin kwenye nyimbo zake, huku akijiita Malkia wa Hip Hop ya Kalenjin.
Nyimbo zake zilizovuma wakati huo ni ‘Hello’ na ‘Utatii’, huku Khaligraph ambaye ni msanii mkubwa wa Hip Hop akiongeza kasi ya mwanadada huyo ya kukua kama mwanamuziki, kupitia kushirikiana naye.
Wengi wahakumwaminia binti huyo alipochipuka hasa kutokana na matamshi yake anapozungumza kwani ameathiriwa na lafudhi ya lugah ya mama.
Mrembo huyo alipunguza sana kazi yake kama mwanamuziki na kuhamia Marekani mwaka 2020, kufuatia changamoto katika mahusiano yake.
Anaishi huko New York na amewahi kuelezea wazi changamoto alizokutana nazo mwanzo baada ya kuhamia Marekani kabla ya kuzoea maisha huko.
Yeye na mpenzi wake ambaye ni mwanajeshi huko Marekani walifunga ndoa rasmi mwisho wa mwaka 2022, katika sherehe ya harusi ya kiraia.