Watu wanaoishi kwenye kingo za mto Tana na maeneo mengine yaliyo chini katika kaunti ya Garissa, wameshauriwa kuhamia nyanda za juu na kuzingatia tahadhari kuhusu mafuriko zinazotolewa kupitia vyombo vya habari kabla ya kuanza kwa mvua ya El Nino.
Akizungumza na wanahabari baada ya kuongoza kikao cha kamati tekelezi ya kaunti hiyo, kamishna wa kaunti ya Garissa Solomon Chesut alisema serikali inajizatiti kuepusha maafa, uharibifu wa mali na kuenea kwa magonjwa yanayoambukizwa kupitia maji.
“Jinsi mnavyofahamu, kaunti ya Garissa ni eneo lililo chini, hasaa katika eneo la mto Tana. Wakati mwingine mto Tana ni baraka kwetu lakini wakati kiwango cha mvua kinapita kiasi, janga hutokea,”alisema Chesut.
Chesut aliyeambatana na washirika na washikadau kadhaa, alifichua kuwa serikali imesambaza rasilimali zote muhimu zitakazohiitajika wakati wa dharura.
Mkurugenzi wa Kaunti anayehusika na mipango maalum Mohamed Dubow alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo, iko tayari kukabiliana na hali yeyote itakayoibuka.
Kaunti za Garissa, Marsabit, Turkana, Baringo, Samburu, Wajir, Tana River, Kwale, Taita-Taveta, Mandera, Narok, na Isiolo, huenda zikashuhudia mafuriko, huku kaunti za Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi zikikumbwa na hatari ya kuathiriwa na maporomoko ya ardhi.