Tume ya Mishahara na Marupurupu nchini, SRC imetangaza kwamba imesitisha mipango yote ya kuongeza mishahara ya maafisa wa serikali katika mwaka wa matumizi ya fedha za serikali wa 2024/2025 hadi itakapotangazwa tena.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari leo Alhamisi, tume hiyo imeelezea kwamba imelazimika kuchukua hatua hiyo kufuatia ukosefu wa fedha unaotokana na kutupiliwa mbali kwa mswada wa fedha wa mwaka 2024.
Sababu nyingine kulingana na taarifa hiyo ni kupunguzwa kwa ufadhili wa serikali kwa asasi mbalimbali kufuatia kuondolewa kwa mswada huo.
“Uamuzi huu umechochewa na hatua ya serikali kukosa kutenga fedha za kufanikisha nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa serikali, nyongeza ambayo ingeanza kutekelezwa Julai 2024,” ilisema taarifa ya SRC.
Wakati huohuo, SRC inaendelea kusema kwamba iliafikia uamuzi huo baada ya mashauriano na Wizara ya Fedha kwa kuzingatia kanuni zilizoko kwenye kifungu nambari 230 sehemu ya tano ya katiba ya Kenya ya mwaka 2010.
Hata hivyo, SRC imeelezea kwamba nyongeza ya kila mwaka ya mishahara iliyoafikiwa kwa ushauri wake itaendelea kutekelezwa kwa kuzingatia uwepo wa pesa.
Fedha za ziada za kutekeleza utathmini wa majibu ya ukaguzi wa kazi katika mwaka wa 2024/2025 hazitatolewa huku mashirika ya kiserikali yaliyo na makubaliano ya pamoja ambayo yameathiriwa na kusitishwa kwa nyongeza ya mishahara yameshauriwa kurejelea mashauriano na vyama husika vya wafanyakazi.
Tume hiyo imeahidi kuendelea kuchunguza hali ilivyo nchini ili kuweza kutekeleza nyongeza ya mishahara.