Spice Diana aridhia shinikizo za mashabiki wake

Mashabiki wamekuwa wakimsihi afute wimbo uitwao "Gwokute Gwobba" kutoka kwenye akaunti yake ya You Tube.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Diana Hajara Namukwaya maarufu kama Spice Diana hatimaye ameridhia shinikizo za mashabiki wake mitandaoni za kufuta wimbo kwenye akaunti yake ya You Tube.

Mashabiki hao wamekuwa wakimsihi mrembo huyo afute wimbo uitwao “Gwokute Gwobba” ambao ni marudio ya wimbo ambao uliimbwa na mwanamuziki Uncle Chumi na walishirikiana naye.

Wimbo huo ulitolewa mwezi Machi na ukapata maelfu ya mitazamo lakini tangu mwanzo wa wiki hii, mashabiki wa Spice Diana wamekuwa wakitaka aufute wakidai Chumi amemkosea heshima.

Uncle Chumi amesikika katika mahojiano na wanahabari mbali mbali akijigamba kwamba hakutaka kushirikiana na Spice Diana, kwenye wimbo huo.

Kulingana naye, meneja wa Spice aitwaye Roger Lubega ndiye alimlazimisha ashirikiane naye kwenye wimbo huo.

Usemi wa Chumi ulimshangaza Spice Diana, ambaye ameelezea jinsi amekuwa akimjali Chumi kiasi cha kumkaribisha nyumbani kwake.

Kabla ya kuingilia tasnia ya muziki, Spice Diana alikuwa muigizaji na alifanya kazi na kundi la Equator Production huko Luzira.

Wimbo wake wa kwanza uliopokelewa na wengi ni “Onsanula” ambao uliandikwa na kuandaliwa na Dkt. Fizo. Kampuni ya Equator Production ilihusika katika maandalizi ya video ya wimbo huo.

Website |  + posts
Share This Article