Mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz yuko nchini Uganda ambapo alitumbuiza kwenye tamasha la Kahawa ambalo pia liliambatana na mashindano ya mbio.
Diamond alifika katika eneo la Rwashameire in Ntungamo jana Jumamosi Mei 24, 2025 asubuhi ambapo alitarajiwa kutumbuiza pamoja na wasanii kama Bebe Cool, Eddy Kenzo, The Ben wa Rwanda, Ray G, Truth 256 na wengine.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Diamond alisifia mipangilio ya tamasha hilo ambalo limeandaliwa na Inspire Africa Group na kufadhiliwa na benki ya Equity.
Diamond alihusika katika shughuli ya upanzi wa miche ya mikahawa katika shamba ambalo liko karibu na ufuo wa ziwa Nyabihoko.
Ufuo huo unaundwa kuwa kivutio cha kilimo cha kahawa na umezingirwa na mashamba ya kahawa na una vyumba vya wageni kulala na uwanja mdogo wa ndege.
Bebe Cool ambaye anajiandaa kuzindua albamu yake Mei 30, 2025 alisema mradi huo unafaa kuwa msukumo kwa raia wa Uganda kwamba mabadiliko ya kiuchumi yanawezekana.
Alifurahia kuhusika katika mipango inayolenga kuinua kilimo cha kahawa akisema kahawa ya Uganda inapofanya vyema ulimwenguni katika mauzo, Uganda inafanya vyema.
Wanariadha walianzia mbio zao katika eneo hilo la Rwashameire na kumalizia huko huko.