Murkomen asema Serikali itakabiliana na majangili Kerio Valley

Alisema hayo kufuatia mauaji ya Padri wa kanisa katoliki Alloys Cheruiyot Bett siku ya Alhamisi katika eneo la Tot, katika bonde la Kerio.

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen amesema kwamba serikali imeongeza juhudi za kuwasaka majangili ambao katika siku za hivi maajuzi wamekuwa wakiua raia wasio na hatia katika eneo la bonde la Kerio.

Matamshi yake yanafuatia mauaji ya Padri Alloys Cheruiyot Bett siku ya Alhamisi katika eneo la Tot, katika bonde la Kerio.

Akizungumza alipozuru familia ya marehemu Padri Alloys nyumbani kwao katika kijiji cha Cheplasgei, huko Kilibwoni kaunti ya Nandi waziri huyo aliapa kuwasaka wahusika wa mauaji hayo.

Murkomen alisisitiza kuhusu kujitolea kwake kuhakikisha usalama kote nchini akisema hakuna yeyote atakayesaazwa.

Alizitaka jamii za kaunti ndogo ya Kerio na eneo zima kushirikiana kikamilifu na maafisa wa usalama ambao wanajitahidi kuondoa wahaifu kati yao.

Murkomen aliwasilisha ujumbe wa pole kwa wazazi wa Alloys ambao ni Eunice na Joseph Binder, kaka na dada zake, kanisa, waumini wa kanisa la mtakatifu Matthias Mulumba parokia ya Tot na jimbo zima la kanisa katoliki la Eldoret.

Wakati huo huo viongozi wa kaunti ya Pokot Magharibi wamelaani mauaji ya Padri huyo katika eneo la Tot ambalo walitaja kuwa hatari zaidi katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Viongozi hao wanaojumuisha Gavana wa Pokot Magharibi Simon Kachapin, mbunge wa Sigor Peter Lochakapong, wa Kapenguria Samuel Moroto na mwakilishi wa kike wa kaunti ya Pokoto Magharibi Rael Kasiwai Aleutum wameitaka serikali kupitia wizara ya usalama wa taifa ichukue hatua dhidi ya majangili wanaochafua amani na usalama wa Kerio.

Website |  + posts
Share This Article