Serikali ya jimbo la Delta nchini Nigeria imetangaza kwamba maafisa wa polisi wamekamata watu 6, kuhusiana na tamasha lililozua ghadhabu mitandaoni la Ozoro.
Tamasha hilo huwa linahusisha hatua ya wanawake kusalia majumbani muda wote huku wavulana na wanaume wakizurura mitaani.
Wanawake ambao hupatikana nje wakati wa tamasha hilo huadhibiwa vikali na wanaume lakini wakazi wengi wa eneo hilo wanafahamu hilo kwa hivyo wanawake hujizuia kabisa kutoka nje.
Lakini mwaka huu, mambo yamekuwa tofauti kidogo ambapo matendo ya tamasha hilo yaligeuka na kuwa dhuluma dhidi ya wanawake.
Hii ni baada ya video ya mojawapo ya matukio ya tamasha hilo kuchapishwa mitandaoni. Inaonyesha mabinti wakishambuliwa na wanaume ambao wanachana nguo zao na hata kuwabaka.
Omorede Sunday anayeaminika kuwa mwandalizi wa tamasha hilo anaripotiwa kuwa mmoja wa wale ambao wametiwa mbaroni.
Kamishna wa polisi katika jimbo la Delta aliona video hizo na kuagiza uchunguzi kuhusu visa hivyo huku akiwataka wananchi walio na taarifa zaidi kuzitoa kwa polisi.
Msemaji wa kamishna huyo Bright Efe alisema kwamba wamejitolea kuchunguza, kukamata wahusika wote na kuwachukulia hatua za kisheria.