Simu 417 zilizoibwa zapatikana kaunti ya Nyeri

Tom Mathinji
2 Min Read
Simu zinazoaminika kuwa zilibwa zapatikana Nyeri.

Maafisa wa polisi wa kitengo cha makosa ya jinai katika kaunti ya Nyeri, wamepata simu za rununu 417 zinazoshukiwa kuibwa, huku mshukiwa mwenye umri wa miaka 32 akikamatwa.

Upatikanaji wa simu hizo ulijiri baada ya kuhojiwa kwa wanaume wawili wenye umri wa makamu waliokamatwa awali na maafisa wa DCI mjini Nyeri.

Kulingana na idara ya upelelezi wa makosa ya jinai katika mtandao wa X, Vijana hao walikamatwa wakiwaibia wafanyabiashara rununu zao katika eneo la Gatitu, Kaunti ya Nyeri.

DCI ilisema kuwa John Kariuki na James Thuita walikamatwa tarehe moja mwezi Novemba mwaka huu, na baada ya kuhojiwa waliwaelekeza maafisa wa polisi katika kituo cha kibiashara cha Gatitu na kumfumania David Thinwa Ngatia ambaye anamiliki duka la kukarabati simu zilizoharibika.

David Thinwa Ngatia anasemekana kuwa mhusika katika sakata hiyo ya wizi wa simu za rununu.

Maafisa hao wa DCI walipata bidhaa zingine zinazoaminika kuwa za wizi zikiwemo runinga mbili, vipakatalishi vitatu, simu, na mashini za chapa miongoni mwa bidhaa zingine. Bidhaa hizo zitatumika kama ushahidi.

Wananchi wametakiwa kuwa makini na kutunza bidhaa zao ipasavyo. Idara ya upelelezi wa maswala ya jinai-DCI imewahakikishia wananchi kuwa imejitolea kushughulikia tatizo la wizi wa simu na itaendelea kuwasaka watu wanaohusika na wizi wa simu.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article