Simple Boy asaka ubalozi wa NACADA

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki Stevo Simple Boy angependa kuhudumu kama balozi wa Shirika la Kupambana na Matumizi ya Mihadarati Nchini, NACADA.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hakimiliki za Muziki Nchini, MCSK Dkt. Ezekiel Mutua alifichua hayo kwenye ukurasa wake wa Facebook muda mfupi baada ya mkutano kati yake na msanii huyo.

“Nilipokutana na Stevo Simple Boy alibainisha wazi anachotaka, kuwa balozi wa mpango wa kampeni dhidi ya matumizi ya mihadarati,” aliandika Mutua.

Mutua aliendelea kuelezea kwamba alimtafuta Mkurugenzi Mkuu wa NACADA Profesa John Muteti kwenye simu na akaridhia kumpa miadi ili kujadili suala hilo.

Kulingana na Mutua, Profesa Muteti alifurahishwa na ari ya mwimbaji huyo wa wimbo, “Vijana Tuache Mihadarati” kutumia talanta yake kuhamasisha vijana dhidi ya matumizi ya mihadarati.

“Nia yetu ni kuwapa vijana matumaini na kuwaunganisha na fursa zilizopo,” aliendelea kusema Mutua kwenye ujumbe wake huku akisema aliridhika kuona kwamba alikuwa amemsababishia Simple Boy tabasamu.

Mwanamuziki huyo ameangaziwa sana siku za hivi karibuni kutokana na ufukara na analaumu uliokuwa usimamizi wake kwa kutowajibika.

Usimamizi huo uliamua kukatiza uhusiano na msanii huyo na sasa anajisimamia kwa usaidizi wa marafiki.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *