Siasa za ukabila hazitakubaliwa nchini, aonya Ruto

Rais Ruto amewataka Wakenya kuepukana na viongozi wanaoeneza siasa za chuki na ukabila na badala yake kuishi kwa amani kwa ajili ya kukuza maendeleo nchini.

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto amewaonya vikali viongozi wanaoeneza siasa za ukabila nchini akisema watakiona cha mtema kuni. 

Badala yake, Ruto amesema kuna haja kwa Wakenya kuishi pamoja kwa amani na kushikana mikono ili kuendeleza nchi kwani umoja wao ni nguvu.

“Unajua kwa hii siasa, kuna viongozi wako na kasumba na pepo ya ukabila na chuki ya kugawanya watu. Mimi nimewaambia hawa viongozi wa pepo chafu ya ukabila na watu wa migawanyiko, wapotee wakipotea. Hii Kenya tunataka tutembee pamoja,” alisema Rais Ruto wakati akiwahutubia wakazi wa kaunti ya Busia.

“Mimi nimewapatia ilani, wale viongozi wote wa ukabila, nyinyi nafasi hamna tena katika taifa letu la Kenya. Hiyo pepo yenu ya ukabila na chuki, hamuwezi kusambaza katika taifa letu…Mimi nikiwa kiongozi wa taifa letu la Kenya, siwezi kukubali viongozi wenye pepo ya ukabila na chuki watugawanye kama taifa letu la Kenya.”

Wakati akiwa ziarani Busia, Rais Ruto alizindua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja ujenzi wa uwanja wa Busia aliosema utakuwa tayari kufikia mwezi Disemba mwaka huu.

Aidha, alizindua ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 15 za Matayos-Nangina na Nangina-Sio Port-Mumbaka ambazo zinajengwa kwa gharama ya shilingi milioni 773.

 

Share This Article