Serikali kwa mara nyingine imetoa wito kwa Wakenya walioko nchini Lebanon kujisajili ili kusaidia katika uhamishaji wao haraka iwezekanavyo.
Wito huo unakuja wakati Israel ikiendelea kutekeleza mashambulizi makali nchini humo kwa lengo la kuwaangamiza wanamgambo wa Hezbollah.
“Tuna mashaka makubwa kwamba idadi kubwa ya Wakenya nchini Lebanon bado hawajajisajili ili kuhamishwa licha ya miito yetu ya mara kwa mara ya kuwataka kufanya hivyo,” imelalama Idara ya Mambo ya Nje katika taarifa.
“Ili kuhakikisha usalama na uhamishaji wa haraka wa raia wetu wote, tunatoa wito kwa Wakenya nchini Lebanon kujisajili nasi mara moja. Ni Wakenya waliojisajili pekee watakaohamishwa.”
Kulingana na taarifa hiyo, serikali tayari imeyahamisha makundi mawili ya Wakenya kutoka nchini Lebanon, na kwamba imejitolea kuendelea na zoezi hilo hadi Wakenya wote walioko nchini Lebanon warejeshwe humu nchini.
Serikali inasema makataa ya Wakenya hao kujisajili ni Oktoba 12, 2024.
Umoja wa Mataifa, UN unasema hadi kufikia sasa, watu wapatao milioni moja wameachwa bila makazi kutokana na vita nchini Lebanon.
Wale wanaotaka kuhamishwa wanapaswa kujisajili kupitia https://www.diaspora.go.ke/lebanon.html, au idara ya mawasiliano na uratibu kupitia nambari ya simu +96590906719, +96171175006 au +254114757002.