Wizara ya Kilimo imewahakikishia wakulima kwamba kuna mbolea ya kutosha, na kuondoa hofu iliyoibuliwa awali kuhusu upungufu wa bidhaa hiyo.
Katibu katika wizara hiyo Dkt. Kipronoh Ronoh, amesema maafisa wa wizara ya kilimo walizuru eneo la North Rift na kubainisha kuwa mchakato wa usambazji mbolea ya bei nafuu, unatekelezwa bila changamoto zozote.
Huku akijibu madai yaliyoibuliwa kuhusu upungufu wa mbolea ya gharama nafuu, katibu huyo alisema ongezeko la hitaji la mbolea hiyo katika maghala ya NCPB, lilisababisha mbolea hiyo kununuliwa kwa wingi lakini mbolea zaidi kwa sasa zinasambazwa kwa NCPB kuhakikisha wakulima wote wanafaidika.
“Ongezeko la hitaji la mbolea ya bei nafuu katika maghala ya NCPB, kutokana na kuanza kwa msimu wa upanzi lilisababisha mbolea hiyo kununuliwa kwa wingi,” alisema Dkt. Ronoh.
Baadhi ya maeneo ambayo maafisa hao wa wizara walizuru kutathmini mchakato wa usambazaji wa mbolea ya gharama nafuu ni pamoja na kituo cha Kaptarakwa, Chama cha ushirika cha Chepkorio kilicho eneo la Elgeyo Marakwet, na chama cha ushirika cha Tuiyotich kilicho katika kaunti ndogo ya Moiben.
Maeneo hayo ni muhimu katika uzalishaji wa chakula kama vile viazi, maharagwe, mboga na matunda, mahindi, mtama, ngano na kahawa.
“Ziara hii ya ukaguzi ni muhimu katika kuwasaidia wakulima, kuimarisha mbinu mbora za kilimo na kufanikisha usambazaji wa mbolea ya gharama nafuu,” ilisema wizara hiyo.