Serikali yatoa shilingi bilioni 4.6 za Inua Jamii

Martin Mwanje
1 Min Read

Serikali imetoa shilingi bilioni 4.6 zitakazosambazwa kwa wazee na watu wenye ulemavu 1, 151, 917 waliosajiliwa kwenye mpango wa Inua Jamii. 

Katibu katika Idara ya Ulinzi wa Jamii na Masuala ya Wazee Joseph Motari amesema kwenye taarifa kuwa fedha hizo ni za mwezi Juni na Julai mwaka huu.

Malipo kwa watakaonufaika yalianza kutolewa leo Alhamisi huku kila mnufaikaji akipokea jumla ya shilingi 4,000 kwa kipindi hicho cha miezi miwili.

“Malipo ya mwezi Juni yalikawia kwa sababu ya zoezi la uondoaji data,” alisema Motari.

“Idara hii inaomba msamaha kwa wanufaikaji kwa usumbufu wowote uliosababishwa na ukawiaji huu.”

Wanufaikaji hulipwa shilingi 2,000 kila mwezi ili kujikimu kimaisha.

Mpango wa Inua Jamii unawalenga watu wenye mahitaji maalum katika jamii ikiwa ni pamoja na wazee wenye umri wa miaka 70 na zaidi , watoto mayatima na wasiojiweza na watu wanaoishi na ulemavu.

Website |  + posts
Share This Article