Wizara ya Elimu imepuuzilia mbali madai ya Baraza la Maaskofu wa kanisa katoliki hapa nchini, kwamba mtaala wa elimu wa CBC unaelekea kusambaratika huku utata zaidi ukizidi kukumba mfumo mpya wa ufadhili wa vyuo vikuu.
Katika taarifa, waziri wa elimu Julius Migos alitetea utekelezaji wa mfumo wa CBC akiongeza kuwa ujenzi wa madarasa 16,000 yanayohitajika kwa wanafunzi wa gredi ya tisa unaelekea kukamilika.
Alisema kuwa serikali imetenga shilingi bilioni 17.6 za kuwezesha kukamilisha madarasa hayo ifikapo Desemba mwaka huu.
“Serikali imechukua hatua madhubuti na kuwekeza kuhakikisha malengo ya mfumo wa CBC yanatimizwa, kupitia utekelezwaji shwari,” alisema waziri huyo.
Waziri alisema kuwa serikali imeajiri walimu elfu 56,950 kwa Shule za Junior secondary huku walimu 46,000 wakitarajiwa kuajiriwa kwa masharti ya kudumu ifikapo Januari mwakani, pamoja na walimu wengine 20,000 wapya.
Alisema kuwa serikali hutoa shilingi 15,042 kwa kila mwanafunzi wa Junior Secondary kila mwaka.
Alisema Serikali imechukua hatua madhubuti na kuwekeza kwa kiasi kikubwa ili kuhakikisha kuwa malengo ya CBC yanaafikiwa kikamilifu.
Kuhusu ufadhili wa vyuo vikuu, Migos alidokeza kuwa mfumo huo mpya tayari umetoa shilingi bilioni 41 kama mkopo tangu mwaka 2023, ambazo zimesaidia vyuo hivyo kujinasua kutoka lindi la madeni.
“Tunawasihi maaskofu wa kanisa katoliki kutopinga mfumo mzima wa elimu, ambao una takriban wanafunzi milioni 11,” alisema waziri Migos.