Wanachama wa kamati ya bunge kuhusu nyumba, mipango ya miji na ujenzi wameitaka serikali kupitia kwa idara ya nyumba na maendeleo ya miji, kuhakikisha kwamba inapokea maoni ya wananchi kuhusu ujenzi wa masoko ya kisasa kabla ya kuanza.
Wakizungumza walipozuru eneo la ujenzi wa soko la Gikomba wanachama hao wakiongozwa na mwenyekiti Johana Ng’eno walisisitiza haja ya kujadiliana na wanabiashara kufahamu majengo faafu kwa bidhaa zao.
“Ni lazima utimize mahitaji ya wanabiashara mbalimbali. Lazima uwasikilize kwa sababu wao ndio watumizi wa masoko hayo.” Alisema Ng’eno.
Mwenyekiti huyo aliongeza kwamba kama kamati, hawataidhinisha miradi ambayo haijapitia mchakato mzima unaofaa huku wanabiashara wakilalamikia ujenzi wa masoko yaliyo wazi wakihofia usalama wa bidhaa zao.
Mbunge wa eneo la Bobasi Innocent Obiri naye alisisitiza haja ya kutanguliza mahitaji ya watakaotumia masoko hayo kabla ya kuangazia muundo.
Kamati hiyo sasa inaelekeza idara ya nyumba na maendeeo ya miji na mkandarasi kuhakikisha vyumba kwenye masoko hayo vina makabati ya kufungwa, huduma za umeme za kutegemewa, maeneo ya kumemesha na mataa faafu ili kuhakikishia wanabiashara usalama.
Kamati hiyo ilizuru pia miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na masoko ya maeneo ya Starehe, Ruiru, Witeithie, Thika Bustani, King Boma Orchard, Thika Depot na Ngoigwa.
