Binti ya Sonko alalamikia ufichuzi unaomhusu

Marion Bosire
1 Min Read
Saumu Mbuvi, mwanawe Gavana wa zamani wa Nairobi, Mike Mbuvi

Binti ya Gavana wa zamani wa kaunti ya Nairobi Mike Mbuvi Sonko aitwaye Saumu Mbuvi amelalamikia alichofichua babake kumhusu.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, Saumu ambaye ni mama ya watoto wawili alisema aliumizwa sana na mambo yaliyosemwa kumhusu na watu ambao anawapenda sana.

“Mengi yamesema kunihusu, mambo ambayo yanaumiza sana, hasa kwa sababu yalisemwa na watu ninaowapenda. Nimeitwa majina, nimehukumiwa na kukosa kueleweka na wengi ambao hawajataka kufahamu ninavyoendelea” aliandika Saumu.

Aliendelea kwa kukiri kwamba ameugua ugonjwa wa “bipolar” alivyofichua babake kwenye mazishi ya mwanahabari Kimani Imbugua akisema hali hiyo imemtesa sana kwa namna ambayo maneno hayawezi kuelezea.

Saumu wakati huo huo alifafanua kwamba tofauti na Kimani, yeye hajawahi kukabiliwa na tatizo la uraibu wa mihadarati na hajawahi kupelekwa kwenye kituo cha urekebishaji.

“Nilitafuta huduma za afya ya akili, sio kwa sababu nilikuwa mraibu, bali ni kwa sababu nilikuwa ninajitafuta tena.” Aliandika msichana huyo.

Alisimulia jinsi inauma kuaibishwa hadharani kwa kujaribu kupona kutokana na ugonjwa huo, hali inayofanywa kuwa mbaya zaidi inapotizamiwa kwamba anaaibishwa na familia yake.

Saumu hata hivyo aliwatia moyo wale ambao wamejipata katika hali sawia akisema simulizi ya maisha yake sio ya aibu bali ni ya kuishi, ujasiri na imani.

Website |  + posts
Share This Article