Serikali imeanzisha uchunguzi kuhusu madai ya kuwepo kwa mbolea feki katika baadhi ya maghala ya halmashauri ya kitaifa ya nafaka na mazao, NCPB.
Msemaji wa serikali Dkt. Isaac Mwaura, amesema hatua hiyo inalenga kuwachukulia hatua za kisheria watakaopatikana kuhusika katika sakata hiyo.
“Katika muda wa wiki kadhaa zilizopita, kumekuwa na malalamishi kuhusu kusambazwa kwa mbolea feki. Nawafahamisha kuwa uchunguzi unaendelea kuhusu swala hilo kwa lengo la kuwachukulia hatua waliohusika na sakata hiyo,” alisema Mwaura.
Akiwahutubia wanahabari leo Alhamisi, Mwaura alisema uchunguzi wa awali uliofanyiwa mbolea hiyo ghushi na shirika la kukadiria ubora wa bidhaa (KEBS), umebaini kuwa mbolea hiyo haikuwa miongoni mwa mbolea zilizosambazwa kupitia mpango wa mbolea za bei nafuu kuitia halmashauri ya NCPB.
“Hakuna aliyejitokeza kuthibitisha kuwa mbolea hiyo feki ilisambazwa na halmashauri ya NCPB,” alisema Mwaura.
Alisema halmashauri ya nafaka na mazao nchini (NCPB), hadi kufikia sasa imepokea magunia milioni 2.3 ya mbolea na imesambaza magunia milioni 2.1 kwa wakulima.
Kulingana na Mwaura, hadi kufikia sasa wakulima 5,533,898 wamesajiliwa katika mfumo jumuishi wa kilimo.