Serikali imetangaza kusitishwa kwa matangazo yote ya michezo ya kamari yanayopeperushwa katika vyombo vya habari nchini kwa kipindi cha siku 30 zijazo.
Hatua hiyo kali inakusudia kuzuia kamari ambazo zinachukuliwa kama zisizofaa na kulinda makundi yaliyo kwenye hatari ya kuathiriwa na matangazo hayo, hasa watoto wadogo.
Kwenye taarifa, Mwenyekiti wa Bodi ya Kudhibiti na Kutoa Leseni ya Michezo ya Kamari (BCLB) Dkt. Jane Mwikali Makau ametangaza kusimamishwa kwa matangazo ya michezo hiyo leo Jumanne akitaja mashaka yanayoongezeka juu ya kuenea kwa shughuli za kamari na matangazo ya kupotosha.
Dkt. Makau amesema bodi hiyo imebaini kuwepo kwa mwenendo unaotia hofu ambapo kampuni za matangazo ya michezo ya kamari zinanadi kamari kama fursa halali ya uwekezaji na njia rahisi ya kujitajirisha.
Alionya kuwa matangazo ya upotoshaji yanakuwa na athari mbaya za kijamii na kiuchumi kwa watu binafsi, familia na jamii kwa jumla.
Mwenyekiti huyo aidha alielezea mashaka juu ya matangazo yaliyozagaa ya michezo ya kamari katika vyombo vya habari wakati usioruhusiwa kati ya saa 11 alfajiri na saa nne usiku.
Kulingana naye, matangazo hayo yanakuwa na athari kwa watoto wadogo na yanachangia kwa visa vinavyoongezeka vya uraibu wa kucheza kamari.
Ili kudhibiti hali hiyo, BCLB imeagiza kusitishwa kwa matangazo yote yanayohusiana na michezo ya kamari katika vyombo vyote vya habari ikiwa ni pamoja na runinga, redio, mitandao ya kijamii, mabango na ujumbe mfupi.
Kumekuwa na ongezeko la matangazo ya michezo ya kamari katika vyombo hivyo katika siku za hivi karibuni huku ikiripotiwa kuwa wengi wanatumia mamilioni kucheza michezo hiyo na kusababisha hata matatizo ya kiakili kwa wanaopoteza fedha zao baada ya kuambulia patupu.