Serikali imetangaza bei mpya za mafuta zilizopunguzwa ambazo zitatumika kwa muda wa mwezi mmoja ujao.
Lita moja ya petroli imepunguzwa kwa shilingi 7 na senti 21, dizeli kwa shilingi 5 na senti 9 huku bei ya mafuta taa ikipungua kwa shilingi 4 na senti 49.
Katika taarifa kuhusu mabadiliko ya bei za mafuta, mamlaka ya nishati nchini, EPRA ilielezea kwamba bei ya bidhaa hizo kutoka nje iliongezeka.
Bei ya kuagiza mafuta ya petroli iliongezeka kwa asilimia 5.6, ya dizeli ikapungua kwa asilimia 0.76 na ile ya mafuta taa ikaongezeka kwa asilimia 1.65.
Kuanzia usiku wa manane leo Alhamisi, mafuta ya petroli yatauzwa kwa shilingi 199 na senti 19 jijini Nairobi huku dizeli na mafuta taa zikiuzwa kwa shilingi 190 na senti 38 na 188 na senti 74 mtawalia.
Mwezi jana, bei ya mafuta ilipungua kwa shilingi moja pekee.
Mapema leo, Rais William Ruto ambaye anaendeleza ziara ya kikazi katika kaunti ya Kericho aligusia upunguzwaji huo wa bei za mafuta.