Katika juhudi za kuimarisha kilimo cha Majani Chai hapa nchini, serikali imetoa kibali cha kufunguliwa kwa viwanda viwili vya Majani Chai ambavyo ni Embomos na Kiptenden,katika eneo la Konoin,kaunti ya Bomet.
Katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, aliyetoa cheti cha bodi ya Majani Chai nchini kwa wakulima wa eneo hilo ili kutoa fursa kwa ujenzi wa viwanda hivyo, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa serikali kupiga jeki uzalisha wa Majani Chai hapa nchini.
Kulingana na katibu huyo, punde tu ujenzi wa viwanda hivyo utakapokamilika, fursa nyingi zitabuniwa katika eneo hilo pamoja na kufanikisha biashara ya Majani Chai ambayo ni nguzo muhimu katika uchumi wa taifa hili.
Dkt. Ronoh alishiriki mazungumzo na wakulima wa Majani Chai, alipoa toa cheti hicho cha ujenzi wa viwanda hivyo viwili,akiwa ameandamana na Afisa Mkuu Mtandaji wa bodi ya Majani Chai Willy Mutai na wakurugebzi wengine wa bodi hiyo.
Katibu huyo pia aliagiza KTDA kuwarejeshea wakulima fedha zilizokatwa kutoka kwa marupurupu yao ili kulipia mbolea ya bei nafuu, akisema serikali imetoa shilingi bilioni mbili kugharamia mbolea ya bei nafuu.
Alisema serikali inatia bidii kuhakikisha wakulima wanafaidika na kilimo cha Majani Chai kupitia mfumo wa kiuchumi kutoka chini almaarufu BETA.
Uzalishaji majani chai hapa nchini hutekelezwa katika vitengo viwili, ule wa mashamba makubwa ambao ni asilimia 40 na ukuzaji kupitia mashamba madogo ambao ni asilimia 60.
Wakulima wengi wa Majani Chai hapa nchini, hushindwa kukimu maisha yao, kwa kuwa wakuzaji zao hilo wana uwezo wa kununua Majani Chai kwa bei ya chini.
Fauka ya hayo, wakulima wengi wa Majani Chai, hufanya kazi katika mazingira hatari na ambayo sio salama kwa afya yao.
Maeneo ambako Majani Chai hukuzwa kwa wingi ni katika nyanda za juu ya Rifta Valley, eneo la Equator ma mashariki mwa eneo la msitu wa Mau.
Wakulima wa Majani Chai huuza zao hilo katika kampuni za halmashauri ya ustawi wa Majani Chai nchini KTDA, kama vile Kapset, Mogogosiek, Rororok, Kapkoros na Tirgaga katika kaunti ya Bomet.