Serikali ya Tanzania yafafanua kuhusu kisiwa cha Lupita

Imesema hakijauzwa na mwekezaji halali anaweza kuhamisha uwekezaji wake kwa mwekezaji mwingine kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali ya Tanzania, imetoa ufafanuzi kuhusu utata ulioonekana kughubika umiliki wa kisiwa cha Lupita, ambacho kinapatikana kwenye Ziwa Tanganyika.

Katika taarifa rasmi, wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi ya Tanzania ilielezea kwamba ni uwekezaji tu unahamishwa wa kisiwa hicho katika wilaya ya Nkasi Mkoa wa Rukwa na wala hakiuzwi.

Taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii awali kuhusu uuzaji huo, zinazoripotiwa kutoka kwa mwekezaji, Tim Draper aliyetangaza kusudio hilo.

“Kisiwa hiki ni moja ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji chini ya Mamlaka ya Uwekezaji na Usimamizi wa Maeneo ya Uwekezaji (TISEZA) na kimepangishwa kwa Kampuni ya Firelight Safaris Ltd ambayo Tim Draper (Raia wa Marekani) ni miongoni wa wanahisa” ilielezea taarifa rasmi ya wizara.

Kulingana na wizara hiyo ya ardhi, sheria ya ardhi sura ya 113 imeweka utaratibu wa namna wawekezaji raia wa kigeni wanaweza kupata ardhi kwa ajili ya uwekezaji chini ya Mamlaka ya Uwekezaji na Usimamizi wa Maeneo ya Uwekezaji, TISEZA.

Inaelezea kwamba TISEZA ambao ndio Wamiliki kwa mujibu wa Sheria, wamepangisha eneo hilo na kutoa hakimiliki isiyo ya asili kwa Kampuni ya Firelight Safaris Ltd kwa matumizi ya hoteli ya kitalii.

“Hivyo Kampuni ya Firelight Safaris Ltd ni Mwekezaji halali katika eneo hilo na anaweza kuhamisha uwekezaji wake kwenda kwa Mwekezaji mwingine kwa kuzingatia Sheria na taratibu za Nchi,” ilifafanua taarifa ya wizara.

Share This Article