Serikali ya Tanzania imeelekeza wananchi hasa wafanyakazi wa umma kufanyia kazi nyumbani leo Alhamisi Oktoba 30, 2025, kufuatia maandamano yaliyoshuhudiwa nchini humo jana.
Baadhi ya raia wa nchi hiyo walitekeleza kile kilichochukuliwa awali kuwa uvumi tu kuhusu kuandamana siku ya uchaguzi mkuu ambayo ilikuwa jana.
Msemaji mkuu wa serikali Gerishon Msigwa alielekeza kwamba watumishi wote wa umma wasalie manyumbani leo, isipokuwa tu wale ambao majukumu yao yanawahitaji kuwa katika vituo vyao vya kazi.
“Kufuatia angalizo la kiusalama lililotolewa na jeshi la polisi kwa wakazi wa Dar es Salaam, serikali inaelekeza kuwa kesho Oktoba 30, 2025 watumishi wote wa umma wafanyie kazi nyumbani.” alisema Msigwa katika taarifa kwa umma.
Msemaji huyo wa serikali alitoa ushauri kwa waajiri wa sekta ya kibinafsi kuzingatia maelekezo hayo na kuruhusu wafanyakazi wao kufanyia kazi nyumbani.
Msigwa alimalizia kuwataka wananchi ambao hawana ulazima wa kutoka kwenye makazi yao nao wasalie nyumbani na kufanyia shughuli zao huko.
Jana jioni polisi wa Dar es Salaam waliwawekea kafyu wakazi wa jiji hilo ambayo ilifaa kuanza saa 12 jioni ila hawakuelekezwa wakati wa kumalizika kwa kafyu hiyo.
Polisi na wahudumu wengine wa usalama ndio pekee waliruhusiwa kuwa kwenye barabara za jiji hilo kushika doria.
