Kampuni inayotoa huduma za teknolojia kwa serikali ya Singapore, GovTech, ameanzisha programu inayolenga kukutanisha watumishi wa umma katika uchumba.
Programu hiyo kwa jina FirstDate, ni jukwaa jipya la majaribio la uchumba lililoundwa makhsusi kwa watumishi wa umma, lengo likiwa kukabiliana na “uchovu wa kuswipe”.
Inadhamiriwa pia kushughulikia kupungua kwa viwango vya wanaozaliwa nchini Singapore, kwa kutoa njia mpya na salama zaidi badala ya programu za kawaida za kuchumbiana.
FirstDate inapatikana kwa maafisa wa umma ambao hawajaoa au kuolewa, wamefiwa na wenzi wao, au wameachana, wenye umri wa miaka 21 hadi 35.
Jukwaa hilo linatoa kipaumbele kwa usalama na kudumisha mahusiano mazuri kazini.
Watumiaji huingia kwa usalama kupitia Singpass, hivyo kuhakikisha kuwa wasifu wote umethibitishwa kikamilifu. Ili kuzuia hali za aibu kazini, mfumo wa programu unahakikisha kuwa washiriki hawataunganishwa na wenzao kutoka taasisi moja ya serikali.
Badala ya mfumo wa kawaida wa kuswipe wasifu bila mwisho, FirstDate inatumia algoriti iliyotambuliwa kupitia Tuzo ya Nobel. Jukwaa hilo hutoa mtu mmoja tu anayependekezwa kwa kila mzunguko, kwa kuzingatia kwa kina mapendeleo ya mtumiaji.
Kipindi cha usajili kwa ajili ya mpango huu wa kipekee wa majaribio unaoendeshwa na serikali kinafungwa leo, Oktoba 5, 2026.
Ingawa GovTech bado haijaahidi kuufanya mpango huo kuwa wa kudumu au kuupanua kwa umma mpana zaidi, macho yote sasa yanaelekezwa kwenye mpango huu wa kidijitali ili kuona iwapo sayansi ya data inaweza kusaidia kuchochea upendo wa kweli miongoni mwa watumishi wa umma na hatimaye kuongeza kiwango cha uzazi.