Serikali ya kaunti ya Nairobi yatoa taarifa kuhusu jengo lililoporomoka

Marion Bosire
1 Min Read

Serikali ya kaunti ya Nairobi imesema kwamba hakuna aliyefariki au kujeruhiwa katika mkasa wa jengo kuporomoka mtaani Mirema Springs, eneo la Roysambu.

Kwenye taarifa iliyotiwa saini na kaimu katibu wa kaunti Patrick Analo, serikali ya kaunti inadhibitisha kwamba jengo hilo liliporomoka usiku wa manane Septemba 24, 2023.

Mmiliki wa jengo hilo Joseph Wakiri anasemekana kukiuka sehemu ya 16 ya sheria ya ujenzi na matumizi ya ardhi ya mwaka 2019 na amekuwa akikwepa kukamatwa na maafisa husika kwa muda mrefu.

Idara ya mipango ya miji chini ya serikali ya kaunti ya Nairobi ilikuwa imetoa kibali cha ujenzi wa nyumba za makazi zilizo gorofa katika eneo hilo na wakati wa kuporomoka, ujenzi ulikuwa umefikia orofa ya 9.

Serikali ya kaunti ya Nairobi sasa imechukua usimamizi wa eneo hilo na tayari imepeleka sampuli kwa idara ya kitaifa ya kukagua majengo na majibu yanatarajiwa hivi karibuni.

Analo kwenye taarifa hiyo anasema wamedhibitisha kwamba hakuna ushahidi wa kuonyesha ukaguzi wa mhandisi na msanifu mijengo katika eneo hilo la ujenzi.

Aliyepatiwa zabuni ya kutekeleza ujenzi huo alikamatwa na kufikishwa mahakamani. Aliachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu ya shilingi laki 5 ila kwa sasa yuko rumande katika gereza la Nairobi west.

Share This Article