Trump kujadiliana na viongozi wa Mexico na Canada leo Jumatatu

Hii ni baada ya Marekani kuweka ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa zinazoingizwa Marekani kutoka Canada na Mexico isipokuwa bidhaa za nishati kutoka Canada ambazo zitatozwa asilimia 10 kuanzia kesho Jumanne.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Marekani Donald Trump amesema atajadiliana na viongozi wa nchi za Mexico na Canada Jumatatu Februari 3, 2025 baada yake kuwekea nchi hizo iwango vipya vya ushuru.

Serikali ya Trump inapanga kuweka ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa zinazoingizwa Marekani kutoka Canada na Mexico isipokuwa bidhaa za nishati kutoka Canada ambazo zitatozwa asilimia 10 kuanzia kesho Jumanne.

China nayo imewekewa ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa zake zinazoingizwa nchini Marekani.

Kadhalika Trump ametishia kuweka viwango vipya vya juu vya ushuru kwa bidhaa zinazotoka nchi za umoja wa ulaya hivi karibuni.

Waziri mkuu wa Canada anayeondoka Justin Trudeau alisema nchi yake itajibu pia kwa viwango sawia vya ushuru kwa bidhaa za thamani ya dola za Canada bilioni 155 zinazoingizwa humo kutoka Marekani.

Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum naye aliagiza viwango sawa viwekewe bidhaa zinazotoka Marekani hatua ambayo China pia imeahidi kutekeleza ikisema Marekani inakiuka sheria za shirika la biashara ulimwenguni WTO.

Kulingana na Trump uchungu utakaotokana na viwango vipya vya ushuru ambavyo Marekani imewekea nchi hizo na vile ambayo itawekewa na nchi husika ni muhimu huku akikashifu wanaopinga mpango wake.

Ikumbukwe kwamba China, Mexico na Canada ndizo washirika wakuu wa kibiashara wa Marekani, ambapo iliagiza bidhaa za thamani ya dola Trilioni 3.2 mwaka 2022, na hivyo ikawa nchi iliyoagiza bidhaa nyingi zaidi kutoka nje.

Kati ya bidhaa hizo, zilizotoka China ni za thamani ya dola bilioni 536.3, zilizotoka Mexico zilikuwa za thamani ya dola bilioni 454.8 na zilizotoka Canada zilikuwa za dola bilioni 436.6.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *