Serikali ya Bavaria yapiga jeki ajenda ya Bottom-Up

Tom Mathinji
2 Min Read
Naibu Rais Rigathi Gachagua na waziri anayehusika na maswala ya kimataifa na yale ya bara ulaya wa jimbo la Bavaria Bi Melanie Huml.

Ajenda ya Rais William Ruto ya kuboresha uchumi ya Bottom Up imepigwa jeki, baada ya serikali ya eneo la Bavaria, nchini Ujerumani kuunga mkono mipango ya rais ya kubuni nafasi za kazi na kuhimiza uvumbuzi.

Serikali ya jimbo hilo la Bavaria siku ya Jumapili iliijumuisha Kenya katika ushirikiano wake wa kimikakati na bara la Afrika, huku ikiahidi kuunga mkono mpango wa Kenya wa ukuaji endelevu wa uchumi.

Hatua hiyo iliafikiwa baada ya mkutano baina ya naibu wa rais Rigathi Gachagua na waziri anayehusika na maswala ya kimataifa na yale ya bara ulaya wa jimbo la Bavaria Bi Melanie Huml jijini Munich, Ujerumani.

Gachagua, ambaye alikuwa akimwakilisha rais Ruto, alisema serikali ya jimbo la Bavaria imekubali kushirikiana na Kenya katika maswala mbalimbali kama vile biashara kwa vile serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa mataifa ya kigeni.

“Napongeza serikali ya Bavaria kwa ukuaji wa uchumi na kukubali kushirikiana na Kenya. Nilikuwa na mjadala wa kufana na wanabiashara wa Bavaria na tumeweka mikakati ya jinsi tutaendelea kushirikiana kati ya serikali ya Bavaria na Kenya,”alisema Gachagua.

Mazungumzo baina ya Gachagua na Bi Huml pia yaliangazia ushirikiano katika sekta nyingine muhimu kama vile kawi safi, utengenezaji bidhaa, utalii, leba, uhamiaji, ustawi wa michezo, elimu miongoni mwa maswala mengine.

Naibu Rais alikuwa ameandamana na mke wake mchungaji Dorcas Rigathi, mbunge wa Baringo ya kati Joshua Kandie na balozi wa Kenya nchini Ujerumani Tom Amolo.

Share This Article