Serikali imetoa wito kwa wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma wanaogoma kusitisha mgomo wao ulioingia siku 46 leo Ijumaa na kurejea kazini huku mazungumzo yakiendelea juu ya namna ya kuwalipa malimbikizi ya mshahara wao ambao serikali inasema kima chake ni shilingi bilioni 7.76.
Kwenye taarifa, Waziri wa Elimu Julius Ogamba amesema serikali iko tayari kulipa fedha hizo kwa awamu mbili.
“Kufuatia zoezi la uthibitishaji, serikali awali ilijitolea kulipa salio lililothibitishwa la shilingi bilioni 7.76 katika awamu tatu – shilingi bilioni 2.1 katika awamu ya kwanza na bilioni 2.8 katika kila awamu mbili za mwisho. Kwa upande mwingine, vyama vya wafanyakazi wa vyuo vikuu vilitaka malipo hayo kutolewa kwa mkupuo mmoja na kukataa ofa ya serikali,” alisema Waziri Ogamba kwenye taarifa.
“Ikilegeza kamba zaidi hiyo jana, serikali ilijitolea kulipa salio lililothibitishwa katika awamu mbili. Mapema leo, uongozi wa vyama vya wafanyakazi wa vyuo vikuu, kwa bahati mbaya, ulielezea kukataa ofa ya serikali.”
Waziri akisikitikia msimamo huo ikizingatiwa masuala yaliyoibuliwa na vyama hivyo, kulingana naye, yameangaziwa kikamilifu na mchakato wa kuangazia masuala yaliyosalia kuwasilishwa kwa vyama hivyo.
“Kwa hivyo tunatoa wito kwa vyama vya wafanyakazi wa vyuo vikuu kuwa na hisia ya uzalendo na wajibu wa kuwajali wanafunzi wetu, kwamba warejee kazini katika vyuo vikuu vyao husika na kutoa fursa ya mazungumzo yenye tija kuelekea suluhu endelevu na inayokubalika kwa pande mbili,” Waziri Ogamba aliwasihi wahadhiri.
Awali, wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma kote nchini waliapa kuendelea na mgomo baada ya kuazimia kuwa watakubali tu malipo ya malimbikizi yao ya mshahara kwa mkupuo mmoja.
Ingawa serikali inasema inadaiwa na wahadhiri hao shilingi bilioni 7.7, wahadhiri kwa upande wao wanasema fedha wanazodai ni shilingi bilioni 7.9.
Wakiwahutubia wanahabari, maafisa wa vyama vya UASU na KUSU waliibuka leo Ijumaa na kusema baada ya kutafuta ushauri, wanachama hao wamesema kamwe hatawakubali malimbikizi ya mshahara wao kulipwa kwa awamu.
“Wahadhiri wamesema hawatoi elimu kwa wanafunzi kwa awamu,” alisema Katibu Mkuu wa UASU Dkt. Constantine Wasonga wakati akiwahutubia wanahabari.
“Kwa hivyo wanataka fedha hizo zilipwe kwa mkupuo mmoja tena mara moja,” aliongeza Dkt. Wasonga wakati akisisitiza kuwa mgomo wao utaendelea hadi matakwa yao yatimizwe kikamilifu.
Katibu Mkuu wa KUSU Dkt. Charles Mukhwaya akiongeza kuwa shauku ya wahadhiri kukataa kulipwa kwa awamu imetokana na hulka ya serikali kuwachezea shere kila baada ya kuingia kwenye makubaliano siku zilizopita.
Ilitarajiwa kuwa wahadhiri wangekubali malipo kwa awamu mbili na hivyo kusitisha mgomo ambao umelemaza masomo katika vyuo vikuu vya umma kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu.
Ilivyo sasa, itawabidi wanafunzi kuendelea kuhisi makali ya mgomo huo.
Mahakama iliamuru jana Alhamisi kuwa serikali iwalipe wahadhiri wanaogoma malimbikizi ya shilingi bilioni 7.9.
