Serikali kuzindua mipango ya kuimarisha uwiano wa kitaifa

Martin Mwanje
1 Min Read

Serikali kuu inafanya mipango inayolenga kueneza amani katika maeneo mbalimbali kote nchini na pia kuimarisha uwiano wa kitaifa. 

Ili kuhakikisha ufanisi wa mipango hiyo, Katibu katika Wizara ya Usalama wa Kitaifa Dkt. Raymond Omollo leo Jumatatu ameshiriki mkutano na jopo huru la washauri juu ya mipango hiyo.

Jopo hilo linajumuisha mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano, NCIC Samuel Kobia miongoni mwa washauri wengine.

“Ili kujiandaa kwa mipango ijayo ya kitaifa ya kueneza amani, leo asubuhi, niliongoza mkutano wa washauri wa jopo huru,” alisema Dkt. Omollo baada ya mkutano huo.

“Mazungumzo yaliangazia kutambua njia zinazofaa zaidi za kuhakikisha ufanisi wa zoezi hili muhimu, ambalo linalenga kueneza amani na kuimarisha uwiano wa kitaifa.”

Mkutano huo unakuja wakati nchi inakumbana na changamoto za kila aina kiasi kwamba Rais William Ruto ametoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kitaifa kuangazia changamoto hizo.

Mathalan, vijana wa Gen Z wamekuwa wakifanya maandamano ya kushinikiza kutekelezwa kwa mabadiliko muhimu nchini, maandamano ambayo yamekuwa tishio kwa uwiano wa kitaifa.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *