Rais William Ruto amesema kwamba serikali itatoa usaidizi kwa familia za waliopoteza maisha kwenye maandamano nchini.
Akizungumza katika ikulu ya Nairobi wakati wa kutoa orodha iliyokuwa imesalia ya mawaziri, Rais Ryto alitambua kwamba ni haki kwa kila mkenya kuafanya maandamano ya amani na kutoa maoni.
Hata hivyo alijuta kwamba watu walipoteza maisha wakitekeleza haki zao za kikatiba.
“Ni kwa majuto makubwa ninalazimika kusema kwamba wakenya wengi walipoteza maisha na wengine wameachwa na majeraha mabaya kutokana na usumbufu wa wasiozingatia sheria wakati wa maandamano.” alisema Rais.
Kiongozi wa nchi alisisitiza kwamba mwelekeo kama huo haufai katika demokrasia na ni lazima wafanye kila juhudi kuhakikisha matukio hayo hayarejelewi siku za usoni.
Ruto aliwataka wahusika wote wa mfumo wa haki nchini kuhakikisha wasiokuwa na hatia na ambao walikamatwa na kufunguliwa mashtaka wakati wa maandamano wanaachiliwa na kesi zao kufutiliwa mbali.
Alisema hatua hiyo itatoa fursa kwa wahusika hao wa mfumo wa haki nchini kuangazia uchunguzi dhidi ya wahalifu halisi ili wafunguliwe mashtaka ifaavyo.
“Ni muhimu kuhakikisha kwamba wahalifu kama hao wanachukuliwa hatua kulingana na sheria.” alisema Rais kuhusu wahuni waliotumia fursa ya maandamano ya vijana kutekeleza uhalifu.
Alithibitisha jukumu la vyombo vya usalama nchini kulingana na katiba ambalo ni kulinda mali na maisha ya wakenya pamoja na kulinda mipaka ya taifa dhidi ya maadui.
Kutokana na hilo amesihi maafisa wa polisi kutumia mamlaka waliyopatiwa na katiba ipasavyo kwa lengo la kuimarisha malengo ya vifungu nambari 238, 239 na 244 vya katiba.