Serikali kuongeza kiwango cha kahawa kinachouzwa nje ya nchi

Tom Mathinji
1 Min Read
Serikali kuongeza kiwango cha kahawa kinachouzwa nje ya nchi.

Serikali inalenga kuongeza kiwango cha kahawa kinachouzwa katika soko la nje, kutoka metrik tani 51,000 hadi metrik tani 150,000 kufikia mwaka 2027.

Akizungumza leo Alhamisi alipohutubia taifa katika majengo ya bunge, Rais alisema ili kuhakikisha sekta ndogo ya kahawa inanawiri, serikali pia imeongeza kiwango cha malipo kupitia kwa hazina ya Cherry kutoka shilingi milioni 2.7 hadi shilingi milioni 6, huku hazina ya bidhaa ikipiga jeki utoaji huo wa malipo kwa shilingi bilioni 1.5.

Kulingana na kiongozi huyo wa taifa, bei ya kahawa katika soko la kahawa la Nairobi, limeongezeka kwa asilimia 25.

Rais Ruto alisema katika muda wa mwaka mmoja uliopita, taifa hili lilizalisha na kuuza nje ya nchi metrik tani 48,000, huku mapato ya shilingi bilioni 25 yakinakiliwa.

Aidha, Rais alidokeza kuwa magunia 320,000 ya mbolea yametengewa sekta ya kahawa pekee.

Hatua hizo zinalenga kuongeza mapato ya wakulima wadogo kutoka shilingi 300,000 hadi shilingi 500,000 kwa kila ekari kwa mwaka kufikia mwaka 2027.

Share This Article