Makumi ya raia wa Ethiopia ambao walikuwa wamezuiliwa na magenge ya utapeli na kuhangaishwa nchini Myanmar wamerejeshwa nchini kwao.
Mwezi jana, zaidi ya watu 250 kutoka mataifa 20, ikiwemo Tanzania na Kenya ambao walikuwa wakifanya kazi katika vituo vya utapeli na wizi wa mtandaoni katika Jimbo la Kayin, nchini humo waliachiliwa na moja ya makundi ya kijeshi huko Myanmar, na kupelekwa Thailand.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imetangaza kuwa kwa kushirikiana na ubalozi wake ulioko India, raia wake 32 kati ya 133 wamerejeshwa nyumbani, kwa mujibu wa gazeti moja nchini humo.
Serikali ya Ethiopia pia imetoa wito kwa umma kuepuka hadaa zinazotolewa na magenge ya utapeli, ili kuepuka uhamiaji haramu kwenda katika nchi ambazo mikataba ya ajira haina dhamana.
Wafanyabiashara na wamiliki wa vituo ama ofisi hizo hutafuta wafanyakazi wanaojua lugha za wale wanaolengwa kufanyiwa utapeli, udanganyifu au wizi wa mtandaoni, mara nyingi ni lugha ya Kiingereza na Kichina.
Wamekuwa wakiingizwa katika shughuli za uhalifu mtandaoni, kuanzia ulaghai wa mapenzi unaojulikana kama “pig butchering” na wizi wa fedha kwa njia ya mtandao, hadi utakatishaji wa fedha na kamari haramu.
Baadhi yao waliridhia kufanya kazi hii, lakini wengine walilazimishwa kufanya kazi hiyo, na kuachiliwa kwao kunategemea familia zao kulipa fidia kubwa.
Baadhi ya wale waliofanikiwa kutoroka wamesema walikuwa wakiteswa.
Wiki moja iliyopita, Serikali ya Kenya ilitangaza kuwa inajadiliana na serikali ya Thailand ili kufungua tena mpaka wa Thailand na Mnyamar ili kuwahamisha Wakenya 64 waliookolewa kutoka katika mitandao ya magendo ya binadamu nchini Myanmar.
Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora ilifichua kwamba kundi hilo limekwama mpakani na ni miongoni mwa raia wa kigeni zaidi ya 7,000 walioachiliwa na makundi yenye silaha lakini hawakuweza kuvuka kufika Thailand tangu Februari 12, lakini kundi la kwanza la watu 260 wakiwemo Wakenya 23 waliruhusiwa kupita.
“Serikali ya Kenya inashauriana na Serikali ya Thailand ili kivuko cha mpaka kifunguliwe tena kwa misingi ya kibinadamu ili kuruhusu raia waliookolewa kuingia katika eneo la Thailand na kurejeshwa Kenya,” imesema taarifa ya wizara hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la KBC, Wizara hiyo ilisema Balozi wa Kenya nchini Thailand amekuwa akiwasiliana kila siku na raia hao huku maafisa wakitafuta njia mbadala za kuwarudisha nyumbani.
Wakati huohuo, hali katika kambi za kijeshi za muda katika Jimbo la Karen nchini Myanmar ambako waathiriwa wamehifadhiwa ni mbaya kutokana na upatikanaji mdogo wa matibabu, maji safi, umeme na vyoo.