Serikali kuhakikisha afya bora kwa Wakenya wote

Dismas Otuke
1 Min Read

Serikali imekariri kujitolea kuhakikisha Wakenya wote wanapata huduma bora za afya na za bei nafuu.

Hii ni kwa mujibu wa Katibu wa Afya ya Umma Mary Muriuki aliyezungumza leo Jumamosi alipohudhuria siku ya umma ya jamii ya Ismaili.

Muriuki alisema mojawapo ya maazimio ya serikali ya Kenya Kwanza ni kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa urahisi kupitia kwa mpango wa
Afya Bora Mashinani.

Aliipongeza jamii ya Ismaili kwa mchango wake wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kupitia kwa uwekezaji katika sekta za afya na bima nchini.

Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muriuki akiwa katika sherehe za kuadhimisha siku ya umma ya jamii ya Ismaili

Jamii ya Ismaili hutoa huduma za afya kupitia kwa hospitali za Aga Khan zilizo katika maeneo mbali mbali kote nchini.

Muriuki pia alifichua kuwa Rais William Ruto anatarajiwa kuzindua mpango wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, UHC Oktoba 20 mwaka huu wakati wa maadhimisho ya sherehe za siku kuu ya Mashujaa.

UHC inajumuisha nguzo nne kuu za kubadilisha mfumo wa kutoa huduma za afya kuwa wa kidijitali,kufadhili sekta ya afya,kuongeza nguvukazi katika sekta ya afya na usalama wa huduma za afya.

Share This Article