Serikali itaanza kulipia gharama za kujifungua katika hospitali za umma mwezi ujao. Kupitia mpango mpya wa bima ya afya ya umma (SHIF), serikali italipa shilingi 10,000 na 34,200 kwa kujifungua kawaida na njia ya upasuaji mtawalia.
Vile vile, malipo haya yatagaramia siku mbili na tatu kwa kujifungua kawaida na upasuaji mtawalia. Wale wenye shida za dharura za ujauzito pia wamejumuishwa.
Katika hatua hii mpya, Wizara ya Afya imetaja kuwepo kwa aina mbili ya malipo – bima ya afya ya umma ya msingi-PHC na ile ya SHIF. Kwenye bima ya msingi, kina mama na watoto watashughulikiwa pasipo na kujali hali zao za malipo kwa bima katika hospitali ya viwango vya pili na tatu. Hata hivyo, kwa wajawazito, bima ya msingi itagarimia tu wale wanaotibiwa na kurudi nyumbani.
Kando na kujifungua, bima ya SHIF itagarimia ukunga, chumba cha upasuaji, wodi, chumba cha matibabu, chakula na mlo maalum, chanjo ya watoto, uchunguzi wa maabara na usafirishaji wa dawa na vifaa.
Zaidi ya hayo, bima itagarimia wanaopanga uzazi na shida zinazoambatana kama kutokwa kwa damu na matatizo ya watoto wachanga.
Kujifungua kwa kawaida na upasuaji katika hospitali za umma kwa kawaida hugharimu shilingi 10,000 na 28,000. Kwenye hospitali za kibinafsi, gharama huwa ghali na hutofautiana kutegemea kiwango na ubora wa hospitali au zahanati.