Serikali italipa gharama zote za hospitali kwa waathiriwa wa mafuriko katika eneo la Maai Mahiu. Hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa serikali Isaac Mwaura.
Mwaura alikuwa akiwahutubia wanahabari Jumanne mjini Mombasa, ambapo alithibitisha kuwa watu 73 walijeruhiwa katika mkasa huo, na kulazwa katika hospitali zilizo karibu.
Aidha alisema kaunti ya Nairobi ndiyo iliyoathiriwa zaidi na mafuriko yanayoendelea, huku watu 147,000 wakilazimika kuhama makazi yao, ikiwa ni asilimia 77 ya watu wote waliofurushwa makwao nchini.
Serikali imeweka kambi 52 za wakimbizi, ili kuwahifadhi watu walioathirika.
Mafuriko yaliyotokea katika eneo la Mai Mahiu, kufikia sasa yamesababisha vifo vya watu 71 huku wengine 28 wakiwa hawajulikani waliko.
Siku ya Jumanne, baraza la mawaziri liliwataka watu wanaoishi katika maeneo yanayokumbwa na hatari, kuhama katika muda wa saa 48.
Serikali ilisema wale watakaokaidi agizo hilo watahamishwa kwa nguvu, kwa usalama wao.