Serikali kufidia familia zilizoathiriwa na mafuriko, asema Rais Ruto

Tom Mathinji, PCS, PCS and PCS
2 Min Read
Rais William Ruto, azuru waathiriwa wa Mafuriko Mathare, Nairobi.

Serikali itaunga mkono familia zote zilizoathiriwa na mafuriko katika maeneo mbalimbali kote nchini, Rais William Ruto amesema.

Rais alisikitika kuwa mafuriko hayo yamesababisha vifo na uharibifu wa mali kwa maelfu ya Wakenya kote nchini.

Alikuwa akizungumza katika eneo la  Kiamaiko mtaani Mathare, Nairobi, alipozuru eneo hilo siku ya Jumatatu kutathmini hali ya mafuriko na kuwatembelea waathiriwa waliofurushwa na mvua kubwa.

Katika ziara hiyo, Rais Ruto alitangaza kwamba kila familia iliyoathiriwa itapewa pesa taslimu shilingi 10,000, kutafuta makao mbadala kwa muda wa miezi mitatu.

“Tumetambua familia 40,000 zilizoathiriwa na mafuriko Nairobi. Tutaipa kila familia shilingi 10,000,” alisema Rais Ruto.

Alisema familia zilizoathirika zitapewa kipaumbele katika ugawaji wa nyumba 20,000 za bei nafuu, ambazo zitatangazwa hivi karibuni kwa ajili ya ujenzi.

Aliwashukuru Wakenya kwa kutii wito wa serikali kwa walio katika hifadhi za mito kuhamia maeneo salama.

Akisema mabadiliko ya tabianchi ndio yanasababisha hali ya sasa, Rais Ruto amewataka Wakenya kuzidisha upanzi wa miti kote nchini.

Alisisitiza dhamira ya serikali ya kupanda miti bilioni 15 ndani ya miaka 10 ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na athari za ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi.

“Tutashirikiana kwa karibu na mashirika ya kijamii katika kusafisha na kupanda miti kando ya Mto Nairobi,” Rais alisema.

Alidokeza kuwa Shilingi bilioni 1 zitatumika katika ujenzi wa shule mpya na madarasa ambayo yameharibiwa na mafuriko Nairobi.

Website |  + posts
Share This Article