Serikali imejitolea kuhakikisha vyama vya ushirika vinapata mikopo nafuu, huku vikiimarisha uwezo wao wa kudhibiti madeni kikamilifu.
Akizungumza mjini Mombasa wakati wa kongamano kuhusu vyama vya ushirika, waziri wa vyama vya ushirika na ustawi wa biashara ndogo na za kadri Wyclifee Oparanya, alisema mojawepo wa mageuzi yanayotekelezwa ni kubuniwa kwa hazina ya dhamana, kama sehemu ya mapendekezo ya mabadiliko katika sheria ya mashirika ya akiba na mikopo.
Kulingana na Oparanya, hazina hiyo itasaidia pakubwa kulinda akiba za wanachama, kuimarisha udhabiti wa kifedha na kuboresha sekta ya vyama vya ushirika.
Mageuzi mengine ambayo yatatekelezwa ni pamoja na kuunganishwa kwa majukwaa ya utoaji mikopo kupitia mitandao katika vyama vya ushirika, hatua itakayosababisha vyama vya ushirika kutoa huduma za kifedha ambazo ni salama na zinazopatikana hususan katika maeneo ambayo yametengwa tangu jadi.
“Kwa kukumbatia usimamizi bora wa fedha, vyama vya ushirika vitakuwa na uwezo wa kustahimili msukosuko wa soko na changamoto zingine za kiuchumi,” alisema Oparanya.
Wakati huo huo, waziri huyo alidokeza kuwa, ili vyama vya ushirika viwe na ushindani wa kupigiwa mfano, ni sharti vikumbatie mfumo wa dijitali hasaa katika utoaji mikopo kupitia simu za mkononi na majukwaa mengine ya kidijitali.
Aidha alivihakikishia vyama vya ushirika kuwa, serikali itatoa vifaa vya kujikinga dhidi ya uhalifu wa mtandaoni ili kulinda deta na mali ya wanachama.