Rais Ruto akataa kutia saini kuwa sheria mswada wa ukinzano wa maslahi

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto.
Rais William Ruto leo Alhamisi alikataa kutia saini kuwa sheria mswada kuhusu ukinzano wa maslahi wa mwaka 2025, na kuurejesha bungeni kufanyiwa marekebisho zaidi.
 
Kiongozi wa taifa alisema sababu kuu ya kurejesha mswada huo bungeni ni kwamba haujaafiki matarajio ya Wakenya.
 
Akizungumza baada ya kuapishwa kwa Mawaziri na Makatibu 14 wa wizara katika Ikulu ya Nairobi, Rais alidokeza kuwa amejitolea kukabiliana na ufisadi na kuimarisha uwajibikaji kwenye uongozi na uadilifu katika utumishi wa umma.
 
“Ninatarajia Mabunge yote mawili yatadhihirisha uongozi kuhakikisha sheria inabuniwa itakayokabiliana na ufisadi ambao wakati mwingi husababishwa na ukinzani wa maslahi miongoni mwa watumishi wa umma wanaopaswa kuwahudumia wakenya na wala sio maslahi yao,” alisema Rais Ruto.
 
Ruto alirejelea kujitolea kwake kukabiliana na ufisadi huku akitekeleza uongozi unaowajibika na kuhakikisha maadili miongoni mwa watumishi wa umma.

Huku mswada huo ukiangazia pakubwa swala la ukinzani wa maslahi, Rais Ruto alidokeza kuwa marekebisho zaidi yanahitajika ili kuimarisha uwazi na utekelezwaji wake kuwiainisha na maadili ya katiba ya uongozi bora.

Mswada huo ulilenga kubuni mikakati ya kikatiba ili kuwazuia watumishi wa umma kutumia nyadhifa zao kwa manufaa yao ya kibinafsi.

Kupitia mswada huo, watumishi wa umma watahitajika kubainisha maslahi ya kibinafsi, kifamilia, kibiashara na inawazuia kushiriki katika maswala ambapo maslahi hayo yapo.

Aidha mswada huo pia unawazuia watumishi wa umma kufanya biashara na taasisi za serikali.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article