Katika juhudi za kuhakikisha utoshelevu wa chakula hapa nchini, serikali hadi kufikia sasa imewekeza shilingi milioni 500 kwa mradi wa ukzaji chakula kupitia unyunyizaji mashamba maji wa Galana Kulalu.
Waziri wa Fedha John Mbadi amesema ufadhili huo umetekelezwa kwa ekari 1,500 ambapo mazao yake yanatarajiwa kuvunwa wiki ijayo, huku mazao mengine kwenye ekari 1,700 za ardhi zikitarajiwa kuvunwa kufikia mwishoni mwa mwezi huu.
Mbadi aliyasema hayo Jumatano alipozuru mradi wa Galana Kulalu kukagua uzalishaji wa chakula kupitia mfumo wa unyunyizaji mashamba maji, akiwa ameandamana na katibu wa idara ya unyunyizaji mashamba maji Ephantus Kimotho.
Kulingana na Mbadi, awamu ya pili ya mradi huo, itajumuisha ujenzi wa bwawa la maji litakalowezesha unyunyizaji wa maji kwa ekari 200,000, na kufanikisha uvunaji wa hadi magunia milioni 14 ya mahindi kila mwaka.
Kwa upande wake, Kimotho alisema mbali na utoshelevu wa chakula, mradi huo umebuni nafasi nyingi za ajira kwa wakazi wa eneo hilo na umekuza mahusiano na miradi mingine kutokana na uwezo wake wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.