Rais William Ruto amesema kuwa serikali imetimiza ahadi zake kwa wakulima, kwa kutekeleza mabadiliko katika sekta ya kilimo hapa nchini.
Kulingana na Rais, serikali imetengea sekta ya kilimo kiwango kikubwa cha fedha, kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa chakula na kuongeza mapato kwa wakulima.
Rais alisema mpango wa serikali wa utoaji mbolea ya gharama nafuu kwa wakulima, umetimiza malengo ya wakulima kwa kuongeza uzalishaji, na hivyo kupunguza gharama ya chakula na gharama ya maisha kwa jumla.
Akizungumza leo Alhamisi wakati wa maadhimisho ya 9 ya kila mwaka ya siku ya wakulima wa maziwa katika uwanja wa Gitoro kaunti ya Meru, Rais alisema uzalishaji wa mahindi umeongezeka kutoka magunia milioni 44 mwaka 2022, hadi magunia milioni 67 mwaka 2023.
“Uzalishaji wa mahindi, kahawa, Maparachichi, Majani Chai na Macadamia pia umeongezeka. Huo ndio mpango tuliokubaliana kwa sababu mlitaka tusimamie sekta ya kilimo kwa njia bora zaidi,” alisema Rais Ruto.
Rais alisema serikali itaendelea kuwasaidia wakulima na pia itatekeleza mikakati zaidi ya kuongeza uzalishaji na mapato kwa wakulima.
Waliohudhuria maadhimisho hayo ni pamoja na naibu Rais Rigathi Gachagua, Magavana Kawira Mwangaza, Cecily Mbarire na Mohamed Adan Khalif.
Wengine ni mawaziri Mithika Linturi, Simon Chelugui, Prof. Kindiki Kithure, wabunge na wawakilishi wadi.