Serikali imejitolea kuimarisha miundomsingi ya michezo, asema Murkomen

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa michezo Kipchumba Murkomen azuru uwanja wa michezo wa Kirigiti, kaunti ya Kiambu.

Waziri wa michezo, ubunifu na maswala ya vijana Kipchumba Murkomen amesema serikali imejitolea kustawisha miundomsingi ya michezo, akielezea umuhimu wa vifaa hivyo katika ukuzaji wa vipawa.

Akizungumza alipozuru uwanja wa Kirigiti ulioko kaunti ya Kiambu, Murkomen alielezea matumaini kuhusu mipango inayoendelea ya ukarabati wa uwanja huo, ulioanza miaka minne iliyopita.

“Nimeridhishwa na kazi inayoendelea na tunaangazia kukamilisha maeneo muhimu ikiwa ni pamoja na kuweka viti na vifaa vya kiteknolojia,” alisema Murkomen.

Waziri huyo alielezea mipango ya kukutana na maafisa wa Sports Kenya, ili kuafikiana kuhusu tarehe ya kukamilishwa kwa ukarabati wa uwanja huo, kufanyia marekebisho ufadhili wa ujenzi huo na kuidhinisha hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kukamilisha ujenzi huo,” alidokeza waziri Murkomen.

Murkomen alielezea haja ya uwanja huo kujisimamia kifedha, kwa kuleta mapato.

“Kirigiti ina nafasi ambazo zinaweza leta mapato na ninakaribisha sekta ya kibinafsi kushirikiana nasi kuwekeza katika vifaa vya michezo kote nchini,’ alisema Murkomen.

Waziri huyo alikuwa ameandamana na mbunge wa eneo hilo Machua Waithaka na waziri wa michezo wa kaunti ya Kiambu Ali Korar.

Share This Article