Mswada wa Kuwatunza na Kuwalinda Wazazi wa Mtoto (Mswada wa Seneti Namba 29 wa 2023) umejadiliwa na Kamati ya Bunge la Taifa juu ya Ulinzi wa Jamii inayoongozwa na mbunge wa Thika Mjini Alice Ng’ang’a.
Mswada huo umedhaminiwa na Seneta Miraj Abdillahi.
Unalenga kuanzisha mpangokazi utakaohakikisha wasichana wajawazito na wazazi wa mtoto wanapata haki ya kuendelea na masomo wakati wakihakikisha malezi na ulinzi wa watoto wao.
Kamati hiyo ilikuwa na mazungumzo ya kina na wawakilishi kutoka Idara ya Elimu ya Msingi na ile ya Ulinzi wa Jamii na Masuala ya Wazee.
Mazungumzo hayo yaliangazia umuhimu wa kutekeleza hatua zinazolinda haki ya wanafunzi wanaoacha masomo kutokana na sababu kama vile mimba za mapema.
Mazungumzo hayo pia yalipigia darubini vifungu husika katika Sheria ya Watoto ya mwaka 2022.
Seneta Gloria Orwoba anaunga mkono kwa dhati mswada huo. Amesisitiza haja ya dharura ya kulinda haki za wazazi wa mtoto, akitaja unyanyapaa wanaokumbana nao watoto hao shuleni kote nchini.
Amesema shule nyingi huwanyima wazazi wa mtoto fursa ya kupata elimu, hali ambayo mswada huo unalenga kukabiliana nayo kwa kuimarisha vifungu ambavyo havijatekelezwa kikamilifu chini ya Sheria ya Watoto ya mwaka 2022.
Wabunge hao walisisitiza umuhimu wa kuanzisha vituo vya malezi katika njia ambayo itawahudumia watoto ipasavyo kote nchini, kwa kuhakikisha msaada wa kutosha unatolewa na serikali kwa makundi haya yaliyopo hatarini.
Wakati wa mkutano huo, ilikubaliwa kwamba mdhamini wa mswada huo ashiriki mkutano na idara hizo mbili ili kujadili masuala yaliyosalia yanayohitaji kuwianishwa au kufanyiwa marekebisho.
Punde baada ya marekebisho yaliyopendekezwa yatakapomalizika, kamati hiyo itakutana tena kuhakikisha vifungu muhimu vimewekwa ili kulinda wazazi wa mtoto na kuhakikisha haki yao ya kupata elimu kote nchini.