Viongozi wa upinzani wametakiwa kuwaelezea Wakenya sera zao kinagaubaga katika azma yao ya kutaka kumbandua Rais William Ruto madarakani mwaka wa 2027.
Ruto anawatuhumu kwa kucheza siasa za kikabila ili kujinusuru kisiasa.
Akizungumza wakati alipoanza ziara yake ya siku tano katika eneo la Mlima Kenya leo Jumanne, Rais Ruto aliwakosoa viongozi wa upinzani kwa kukimbilia kukosoa utawala wake pasi ya kuwasilisha sera mbadala.
Akizungumza katika shule ya Ng’arachi, kaunti ya Laikipia, kiongozi wa nchi hususan aliwapuuzilia mbali wakosoaji wake kwa kukosa maono bayana katika malengo yao ya kumtema kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Aidha, alitoa wito kwa wakazi wa Mlima Kenya kutokubali kushawishiwa na viongozi wanaocheza siasa za kuwaganya Wakenya kwa misingi ya kikabila akionya kuwa siasa kama hizo zitakuwa mwiba kwa utekelezaji wa maendeleo kote nchini.
Aliyasema hayo wakati akiwa ameandamana na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na viongozi mbalimbali wa Mlima Kenya wakiwemo Mawaziri, Magavana, Maseneta na wabunge.
“Hakuna jamii, kaunti au eneo litakalotengwa na serikali jumuishi. Tunaenda kutembea pamoja kuifanya nchi yetu kuwa jumuishi zaidi, iliyostawi na bora kwa ajili ya wote,” aliahidi Rais Ruto wakati wa ziara hiyo.
Akiwa katika kaunti ya Laikipia, Rais aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 10 katika shule ya msingi na sekondari ya juu ya Nanyuki D.E.B. na baadaye kukagua soko la kisasa la Nanyuki ambalo ujenzi wake utagharimu shilingi milioni 350.
Aidha, kiongozi wa nchi alizuru mradi wa nyumba za gharama nafuu wa Nanyuki katika ziara itakayohusisha ukaguzi wa miradi mbalimbali.
Ziara hiyo katika eneo la Mlima Kenya ni ya kwanza kwa Rais tangu kutengana na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua.
Gachagua amekuwa akifanya kampeni ya kutaka wakazi wa eneo hilo kutengana na utawala wa Kenya Kwanza akidai umesaliti maslahi ya eneo hilo.