Samia Suluhu Hassan ameapaishwa rasmi kuwa Rais wa Tanzania baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika nchini humo Oktoba 29.
Hafla ya uapishaji wake iliandaliwa katika uwanja wa kijeshi jijini Dodoma.
“Mimi Samia Suluhu Hassan naapa kwamba nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitumikia kwa moyo wangu wote, na kwamba nitaihifadi, kulinda na kuitetea katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria iliyowekwa. Ewe Mwenyezi Mungu nisaidie,” aliapa Rais Suluhu wakati maandamano yakirindima nchini humo katika siku za hivi karibuni.
Hafla hiyo ilifuatiliwa na wananchi moja kwa moja kupitia runinga, redio na mitandao yao ya kijamii kwani hawakuruhusiwa kuingia uwanjani yamkini kutokana na machafuko ambayo yameshuhudiwa nchini humo.
Hii inakuwa ni mara ya pili kwa Rais Suluhu kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, baada ya kuchukua madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2021 kufuatia kifo cha Rais John Magufuli.
Suluhu alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 29 baada ya kujizolea asilimia 98 ya kura ambazo viongozi wakuu wa upinzani walizuiwa kushiriki.
Ni hatua iliyozua maandamano yenye ghasia ambapo waandamanaji walikuwa wakilalamikia uhalali wa uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa kitaifa wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu alizuiliwa kufuatia madai ya uhaini huku mwenzake wa ACT Wazalendo akitolewa kwenye kinyang’anyiro kwa misingi ya kisheria.
					
			