Ilikuwa zamu ya wabunge kutoka kaunti ya Turkana kutembelea Ikulu ya Nairobi na kukutana na Rais William Ruto ili kuangazia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kuu katika kaunti hiyo.
Wakati wa mkutano huo, Rais Ruto na wabunge hao walikubaliana kwa kauli moja kufanya kazi kwa pamoja kufanikisha miradi ya maendeleo katika kaunti hiyo.
“Tumekubaliana na viongozi kutoka kaunti hiyo kuharakisha ukamilishwaji wa miradi inayoendelea ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na nyumba za gharama nafuu, nyumba za wanafunzi kuishi, masoko ya kisasa, miundombinu ya uvuvi, na uendelezaji wa barabara na maji,” alisema Rais Ruto alipokutana na viongozi hao leo Jumatano.
“Usalama, amani na uwiano vinasalia viwezeshaji muhimu vya kufungua uwezo kamili wa Turkana na kubuni fursa kwa ajili ya watu wake.”
Wabunge hao wakitumia fursa hiyo kupendekeza miradi ya maendeleo inayopaswa kupatiwa kipaumbele katika kaunti ya Turkana inayofahamika kwa kukumbwa na changamoto kama vile uhaba wa maji na ukosefu wa usalama.
Rais Ruto amekuwa akikutana na watu mbalimbali katika Ikulu ya Nairobi ili kujadili miradi ya maendeleo inayotekelezwa na utawala wake, na jana ilikuwa zamu ya wazee wa vijiji kutembelea ikulu hiyo.