Ruto: Serikali imejenga madarasa 14,000 na kuwaajiri walimu 76,000

Rais Ruto aliyasema hayo leo Jumatatu wakati wa uzinduzi wa shule ya msingi ya Lenana katika eneo bunge la Dagoretti Kusini.

Martin Mwanje
2 Min Read
Shule mpya ya msingi ya Lenana

Serikali ya Kenya Kwanza imejenga madarasa 14,000 katika jitihada za kuimarisha utenda kazi wa mfumo mpya wa elimu na kufanikisha mtaala wa umilisi, CBC.

Na ili kuhakikisha mtaala huo kwa unawafaidi wanafunzi kote nchini, Rais Ruto pia amesema serikali yake imeajiri walimu 76,000 tangu ilipoingia madarakani.

Ameahidi kuwa madarasa zaidi yatajengwa na walimu kuajiriwa ili kuhakikisha mfumo mpya wa elimu unafanya kazi vyema kama ilivyokusudiwa.

Akizungumza katika eneo la Ngando katika eneo bunge la Dagoretti Kusini wakati wa uzinduzi wa shule ya msingi ya Lenana, Rais alisema katika kaunti ya Nairobi pekee, madarasa 500 yamejengwa.

Madarasa hayo yalijengwa kutokana na shilingi bilioni moja zilizotolewa kwa wabunge kuboresha miundombinu ya elimu katika maeneo bunge yao ambapo kila mbunge alipokea shilingi milioni 58.

Alimsifia mbunge wa Dagoretti Kusini John Kiarie kwa kuwa mstari wa mbele kuboresha miundombinu hiyo katika eneo bunge lake akisema kufikia sasa, mbunge huyo amejenga madarasa 6.

Rais anasema katika mwaka ujao wa fedha, atatenga shilingi zingine bilioni moja kwa lengo la kuboresha zaidi miundombinu katika shule za umma huku madarasa 1,220 yakikusudiwa kujengwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Alitumia fursa hiyo kuwasihi wazazi kuwalea vyema wanao ili wasitumiwe na watu wasioitakia nchi mema kuwatusi watu wengine katika mitandao ya kijamii kama inavyoshuhudiwa kwa sasa.

Rais alikuwa ameandamana na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na Kiarie miongoni mwa viongozi wengine.

Aliwaahidi wakazi ujenzi wa masoko zaidi, barabara, maji na utoaji wa huduma za afya zilizoboreshwa.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *